Hatimaye Msemaji wa klabu ya Simba, Haji Sunday Manara atashindwa kumposa mnyange Wema Sepetu, baada ya Shirikisho la n Soka Tanzania (TFF) kupangua tena ratiba ya ligi kuu, kwa kusogeza mbele mchezo wa Azam na Ndanda FC.
Manara (Kushoto), Wema (Kulia)
Mchezo huo uliokuwa umepanga kufanyika Jumamosi ya Februari 4, sasa utafanyika Jumapili Februari 5 ili kutoa nafasi kwa Azam FC kujiandaa vizuri kutokana na timu hiyo kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mamelod Sundowns ya Afrika Kusini, siku ya Jumatano usiku.
Maamuzi haya yamefanyika ikiwa ni takriban siku 10 tangu Msemaji huyo wa Simba Haji Manara atangaze kumposa aliyewahi kuwa Miss Tanzania, ambaye pia ni nyota wa bongo movie Wema Sepetu, endapo ratiba isingepanguliwa tena.
Manara alisema kuwa alikuwa na uhakika kuwa ni lazima ratiba ingepanguliwa tena, mara baada ya TFF pia kupangua tarehe ya mchezo kati ya Simba na Yanga uliosogezwa kutoka Februari 18 hadi Februari 25 huku akionesha kushangazwa na jinsi ambavyo TFF inashindwa kutengeneza ratiba ya uhakika.
Katika taarifa yake aliyoitoa usiku wa Januari 23 mwaka huu, manara alisema "Iwapo Kama ratiba yao ya Ligi kuu na Kombe ila shirikisho haitabadilishwa kuanzia sasa hadi mwisho wa msimu, ntamposa mlimbwende Wema Sepetu, na akikubali ntamuoa, akikataa ntatembea na boxer toka Nyumbani kwangu hadi TFF"
Kwa mabadiliko haya ambayo sasa TFF imeyatanga, ni dhahiri kuwa hakuna ndoa tena kati ya Manara na Wema Sepetu, isipokuwa tu kama atatangaza vinginevyo.
Hii ni sehemu ya taarifa yake ya Januari 23, 2017).....
NDANDA NAO WAGOMA
Licha ya kutangaza mabadiliko hayo, uongozi wa Ndanda FC umetangaza kutotambua mabadiliko hayo kutokana na maandalizi iliyokuwa imekwisha yafanya na kutoa msimamo wake kuwa inatambua kuwa mechi yao na Azam inachezwa siku ya Jumamosi, Februari 4.
Mabadiliko hayo ya ratiba pia yamewagusa baadhi ya wadau na kuhoji kuwa iweje mechi ya kirafiki ambayo haikuwa katika kalenda, ivuruge ratiba ya ligi? Hoja ambayo TFF imetetea na kusema kuwa Azam waliokoa jahazi baada ya vilabu vya Simba na Yanga kugoma kucheza mechi zao na Mamelod Sundowns, hivyo ingeweza kuwa aibu kwa taifa.
"Walichokifanya Azam ni kuokoa jahazi na kutuepusha na aibu baada ya hao waliokuwa wamekubaliana kususia mechi, hivyo wameomba kusongezwa mbele mchezo wao kwa ajili ya kujiweka sawa ikiwa ni pamoja na kutibu majeruhi n.k" Amesema Ahmad Yahya, mwenyekiti wa Bodi ya Ligi.
CHANZO: eatv.tv
Post a Comment
Post a Comment