KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Rogers Siyanga amesema mfumo uliotumika na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda hivi karibuni kutaja majina ya watuhumiwa wa dawa hizo ni tofauti na utaratibu wa utendaji kazi wa kamisheni yake, akieleza watajikita katika kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na sheria.
Aidha, Siyanga amesema licha ya kukabidhiwa majina 97 na mkuu huyo wa mkoa katika jalada lililosomeka, ‘majina 97 ya wauzaji dawa za kulevya wakubwa’ yeye atawachunguza watu hao na kufuata taratibu zote za kisheria katika kuwachukulia hatua, lakini wanasheria wamesema Makonda anaweza kusababisha Serikali kushtakiwa.
“Kutangaza majina si kipaumbele chetu sisi tunazingatia uchunguzi na mahojiano ambayo yanaweza kutupatia taarifa zaidi za wahusika kwani huu ni mtandao wa kidunia,”alisema.
Kauli hiyo ya Siyanga inaweza kutafsiriwa kuwa ni kumkosoa Makonda kwa kutaja majina ya watu 65 akiwahusisha na dawa za kulevya, jambo linalotajwa pia kuwa kinyume cha sheria.
Alisema kimsingi mapambano ya dawa za kulevya yalikuwa yakitaribiwa wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya na sheria husika ilitoa nafasi pia kwa mamlaka mbalimbali kujihusisha na operesheni hiyo hadi kufikisha watuhumiwa mahakani.
Kamishna huyo alisisitiza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya mwaka 2015 wanayoisimamia, kutaja majina si kipaumbele kikuu kwao na kwamba wanazingatia uchunguzi zaidi ili kubaini mtandao mzima wa dawa za kulevya.
Alisema kupambana na dawa za kelevya si jambo rahisi na kuwa wanaohusika na biashara hiyo ni watu ambao kwenye jamii wanaonekana wasafi hivyo ni vema kujipanga.
Alisema suala la watu wanaodaiwa kutumia dawa za kulevya kufikishwa mahamakani limejikita katika pande mbili ambazo ni baada ya mhusika kukataa kutumia, lakini pia inaweza kuwa ni sehemu sahihi ya kumtaka mhusika kuacha na huwekwa katika uangalizi.
Siyanga alitoa wito kwa watumiaji wa dawa za kulevya kutoa ushirikiano ili waweze kuwasaidia kwani ni moja ya majukumu yao.
Kesi ya Manji
Alipotakiwa kueleza ni kwa nini Manji alipelekwa mahakamani alisema kimsingi kesi hiyo haiwahusu kwa sababu ilianza kupitia mamlaka nyingine kabla ya mamlaka yake kuanza kazi.
Mapapa wa dawa za kulevya
Kwa upande mwingine, Siyanga alisema mamlaka yake inatarajia kuzunguka katika magereza mbalimbali duniani na kuzungumza na Watanzania ambao wamehukumiwa kunyongwa na vifungo vya maisha ili waweze kuwataja watu ambao wanawatuma kufanya biashara hiyo.
Alisema kupitia utaratibu huo wanaweza kukabiliana na tatizo hilo huku akibainisha kuwa akitolea mfano mfanyabiashara mkubwa ambaye ni mwanamke amehukumiwa kifungo jela, baada ya wafungwa zaidi ya 40 nchini Ujerumani, kubainisha kuwa yeye ndiye aliwatuma.
Kamishna Siyanga alisema pia mfanyabiashara mwingine mkubwa mwanaume, amehukumiwa kwenda jela mwaka 2010 baada ya kubaini mtandao mzima wa tatizo hilo na kuwa mkakati wao ni kumaliza mtandao zaidi.
“Huyu mwanamke yupo gerezani kati ya Segerea au Keko. Huyu mwanaume pia yupo katika magereza yetu,”alisema.
Alisema Tanzania imekuwa ikikamata hadi tani 1.5, kilo 800, 200, 100, 50 hivyo wapo katika mapamano ya kuhakikisha kuwa hali hii inakabiliwa.
Wanasheria wanena
Wakati Siyanga akieleza hayo, wanasheria wameeleza kwa kuandika ‘majina 97 ya wauzaji wa dawa za kulevya wakubwa, Makonda anaweza kusababisha Serikali kushtakiwa wakisema inawezekana hakuwa anajua anachokifanya.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wanasheria hao walisema kilichofanywa na Makonda kuandika watu hao ni wauzaji, kisheria ni kosa kwani tayari alikuwa amewahukumu wakati yeye hana mamlaka hayo.
“Sijui alitoa wapi uwezo wa kuandika kwamba hao watu 97 ni wauzaji wakati bado hata hawajapelekwa mahakamani, achilia mbali kukamatwa. Nafikiri hakuwa anajua nini anakifanya ile kwenye sheria ndiyo tunaita ‘defamation’ yaani unampa mtu hukumu hata kabla ya kumfikisha Mahakamani:
“Hakuna mahali popote kwenye Katiba ya Tanzania inayompa mtu mamlaka hata Rais ya kumhukumu mtu tofauti na mahakama, hiki ndio chombo kinachoweza kusikiliza kesi, kuitolea ufafanuzi na kutoa hukumu tofauti na hapo unaweza baadaye kushtakiwa kwa kuchafua majina ya watu,”alisema Joseph Kiwanga wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Kauli hiyo iliungwa mkono na Wakili James Marenga ambaye alisema sheria ipo wazi kuwa chombo pekee chenye uwezo wa kuhukumu nchini ni Mahakama na siyo Bunge, Baraza la Wawakilishi wala Serikali Kuu.
“Kilichofanywa na Makonda ni kinyume na sheria na endapo watu hao wakihojiwa na kukosekana na hatia wanaweza kufungua kesi ya madai. Katiba yetu inasema vizuri kabisa katika ibara ya 107 A kifungu kidogo cha kwanza kwamba mahakama ndio yenye mamlaka kisheria ya kusikiliza kesi na kumtia mtu hatiani au baada ya kumkosa na hatia hapo mtu huyo anakuwa hana kosa lolote lililothibitika.
“Sheria ilivyo hata kama polisi wamekamata kundi la mateja wanaotumia dawa za kulevya, au wamefanikiwa kuyakamata majambazi bado hawawezi kukupeleka moja kwa moja Segerea au Ukonga japo wana ushahidi hadi upelekwe mahakamani, upelelezi ufanyike ndio mahakama iseme kama imemkuta na hatia, tofauti na hapo unatuhumiwa tu,”alisema Marenga.
Wakili Marenga alisema kifungu cha 13 cha Katiba kinatoa haki ya mtuhumiwa kusikilizwa kwanza kabla ya kuhukumiwa na kuongeza kuwa kama watu hao hawatokutwa na hatia wanaweza kuidai fidia Serikali, jambo ambalo linaweza kulisabishia hasara Taifa kwa kulipa kundi kubwa la watu.
Kwa upande wake Mhadhiri wa UDSM, Dk James Jesse alisema kilichofanywa na Mkuu wa Mkoa ni makosa kwani alihukumu kabla ya kuwapeleka mahakamani na kwamba kama hana ushahidi wa kutosha dhidi ya watu hao ni rahisi kufunguliwa kesi ya kuchafua majina yao.
Hata hivyo, upande wake Wakili Ufforo Mangesho kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema inawezekana Makonda alikuwa na lengo tofauti na ndiyo sababu ya kuyaita majina hayo ‘wauzaji’ badala ya watuhumiwa huku akijua hana uhalali wa kisheria wa kumhukumu mtu.
“Inawezekana kulikuwepo na kingine nyuma ya vita ya dawa za kulevya kwa sababu ninachoamini Makonda alikuwa anajua kabisa kwamba anavunja sheria kwa kuhukumu majina ya watu hadharani ilihali mahakama zipo na ndio zenye wajibu kikatiba wa kushughulikia kesi na kutoa hukumu,”alisema Mangesho.
Februari 13, Mwaka huu wakati akitangaza awamu ya pili ya kile anachokiita vita dhidi ya dawa za kulevya Mkuu huyo wa Mkoa alimkabidhi jalada hilo kamishna Sianga huku likiwa limeandikwa kwamba ni majina ya ‘wauzaji ’ wa mihadarati hiyo jambo ambalo lilileta tafsiri tofauti miongoni mwa wanasheria wakihoji uhalali wa Makonda kuhukumu.
Jamaa atengeneza ndege YAFANIKIWA KURUKA
Post a Comment
Post a Comment