Aliyekuwa Rais wa Gambia, Yahya Jammeh ameondoka nchini humo baada ya mvutano wa muda kufuatia kushindwa katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliofanyika Disemba Mosi mwaka jana.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ECOWAS, kiongozi huyo aliyeiongoza Gambia kwa miaka 22 alipanda ndege kuelekea nchini Guinea ambapo akifika atasafiri kwenda nchini Equatorial Guinea atakapoishi uhamishoni.
Jammeh alishindwa na kiongozi wa upinzani, Adama Barrow ambaye amekuwa akiishi nchini Senegal na kueleza kuwa atarudi Gambia usalama ukiimarika.
Barrow aliyeapishwa katika Ubalozi wa Gambia nchini Senegal, alisema kuwa akiingia madarakani ataunda tume kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa na Yahya Jammeh katika kipindi cha miaka 22 ya utawala wake.
Rais wa ECOWAS, Marcel de Souza pia ameeleza kuwa wanajeshi waliokuwa wametumwa kutoka nchi wanachama kwenye kumuondoa Jammeh madarakani sasa wataondolewa japo wachache watabaki kuendelea kuimarisha usalama.
Wananchi wa Gambia wamekuwa na hisia tofauti kuhusu kuondoka kwa Jammeh ambapo wanaoaminika kuwa ni wafuasi wake walisikitika kwa majonzi alipokuwa akiwaaga katika uwanja wa ndege huku wengine wakishangili kuamini kuwa ni mwisho wa utawala wa kidikteta uliokuwa hauheshimu haki za binadamu.
Kitu alichoahidiwa Jammeh kuweza kuachia madaraka baada ya kukutana na baadhi ya viongozi wa mataifa mengine bado hakijafahamika.
Yahya Jammeh anakuwa Rais wa kwanza wa Gambia kuondoka madarakani kwa amani tangu walipopata uhuru mwaka 1965.
Post a Comment
Post a Comment