Jaji Kaijage (katikati) akiongea na wanahabari visiwani Zanzibar
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewataka wananchi wanaoishi katika kata 19 zitakazofanya Uchaguzi mdogo wa Madiwani kwa upande Tanzania Bara na Ubunge katika jimbo la Dimani Zanzibar, Januari 22, 2017 wajitokeze kwa wingi kupiga kura
Akizungumza na vyombo vya Habari leo mjini Zanzibar, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Rufaa, Mhe. Semistocles kaijage amesema kuwa maadalizi ya Uchaguzi huo yamekamilika na wananchi wote wenye sifa za kupiga kura katika uchaguzi huo wajitokeze kutimiza wajibu wao wa Kikatiba.
Amesema licha ya kuwepo kwa dosari za hapa na pale zilizojitokeza zikiwemo za ukiukwaji wa Maadili ya Uchaguzi kwa baadhi ya Vyama na wagombea wao, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilichukua hatua za kukemea vitendo hivyo ili kuwezesha Kampeni za Uchaguzi kufanyika kwa Usalama na Amani.
Ameeleza kuwa katika uchaguzi huo jumla ya Wapiga Kura 9,280 wa Jimbo la Dimani Zanzibar wanatarajiwa kupiga kura ili kumchagua Mbunge atakayewaongoza kwa kipindi cha miaka 3 kupitia vituo 29 vya Kupigia Kura katika Jimbo hilo.
Kwa upande wa Uchaguzi Mdogo wa Madiwani katika Kata 19 za Tanzania Bara Wapiga Kura 134,705 walioandikishwa wanatarajia kupiga kura katika vituo 359 ambavyo vilitumika katika Uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Amesema kuwa siku ya uchaguzi Januari 22, 2017 vituo vyote vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni na kufafanua kuwa iwapo wakati wa kufunga Kituo watakuwepo Wapiga Kura katika mstari ambao wamefika kabla ya saa kumi jioni na hawajapiga wataruhusiwa Kupiga Kura.
Jaji Semistocles amesisitiza kwamba mtu yeyote hataruhusiwa kujiunga katika mstari wa Wapiga Kura baada ya saa kumi (10:00) jioni muda ulioainishwa kisheria.
Ameeleza kuwa kwa kila mpiga kura katika jimbo hilo akumbuke kubeba Kadi yake ya Mpiga Kura kwa kuwa Sheria ya Uchaguzi inaelekeza kuwa ili Mpiga Kura aruhusiwe kupiga kura ni lazima awe na kadi ya Mpiga Kura.
“ Naomba ieleweke wazi kuwa Fomu Na. 17 siyo mbadala wa Kadi ya Mpiga Kura, Wapiga Kura ambao wana Kadi ya Mpiga Kura lakini taarifa zao hazimo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Kituoni, hawataruhusiwa kupiga kura” Amesisitiza Jaji Kaijage.
Post a Comment
Post a Comment