Shirika la Viwango Tanzania (TBS), limesema upimaji wa awali wa taulo za kike aina ya Elea, umeonesha bidhaa hiyo haijakidhi viwango na haipaswi kuingizwa sokoni.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu TBS, Profesa Egid Mubofu, alisema hayo kupitia taarifa yake aliyoituma kwa gazeti hili alipotakiwa kueleza endapo wanazitambua taulo hizo ambazo zimekwisha gawiwa katika shule mbalimbali nchini.
“Shirika lilipokea maombi ya kupima pedi zinazotumika zaidi ya mara moja (Re usable pads) kutoka Kampuni ya Malkia ambao ni wazalishaji wa bidhaa za Elea.
“Upimaji wa awali wa bidhaa hii, ulifanyika na matokeo yalionesha haikidhi kiwango cha bidhaa husika ambacho ni TZS 1659:2014, mzalishaji akatakiwa kufanyia marekebisho bidhaa hiyo,” alisema.
Mtengenezaji na mbunifu wa taulo hizo, Jenipher Shigoli alikiri kwamba bidhaa hizo hazijapewa alama ya ubora na TBS.
“Ni kweli nilipeleka bidhaa yangu TBS ikapimwa, lakini sikupewa ‘certificate’ ili nianze kuweka alama ya nembo ya ubora ya TBS, niweze kuzisambaza sokoni.
“Waliniambia kuna vitu natakiwa kuboresha kwa hiyo kama nilivyokueleza awali tunajenga kiwanda Kibaha mkoani Pwani, hivyo natarajia kitakamilika Machi, mwaka huu na nitakuwa tayari nimekamilisha vigezo walivyonitaka kuwa navyo,” alisema.
Post a Comment
Post a Comment