Matukio ya kuvamiwa na kuporwa kwa fedha yamekuwa yakiripotiwa kila kukicha. Idadi kubwa ya wananchi wamekuwa wakivamiwa na kuporwa fedha. Katika matukio hayo wapo ambao wameuawa, kujeruhiwa na wengine kupata ulemavu wa maisha. Kutokana na kushamiri kwa matukio hayo mwandishi wetu amefanya utafiti wa jinsi ya kujiepusha kuingia katika janga hilo.
Usitembee na fedha nyingi.
Unapobeba fedha nyingi unajiweka katika hatari ya kudhurika au hata kuuawa. Mhalifu anapofika kwako anachotaka ni kupata fedha, hivyo kumchelewesha maana yake ni kuhatarisha maisha.
Wahalifu wanaweza kupewa taarifa za wewe kuwa na fedha nyingi wakati fulani, au kutokana na kiwewe wahalifu wanaweza kukugundua kuwa umebeba kiasi kikubwa cha fedha na kukuvamia.
Epuka kubeba fedha nyingi, fanya malipo kwa mafungu kidogokidogo mpaka ukamilishe malipo au ununuzi uliotaka kuufanya.
Hakikisha uko salama
Uhalifu unaweza kutekelezwa mahali popote, hivyo ni vyema kila wakati kuhakikisha mazingira uliyopo ni salama.
Kwa mfano unapohisi kuna mtu anakufuatilia, chukua hatua haraka ya kuondoka mahali hapo na kujisogeza unapoweza kupata msaada.
Fanya malipo kwa kadi, simu
Malipo kwa njia za simu au kadi ni namna mojawapo ya kujikinga kwa sababu wahalifu hawawezi kuwa na muda wa kuchukua fedha iliyopo kwenye simu.
Wahalifu wanahitaji fedha za haraka ambazo haziwezi kuacha alama ya wao kukamatwa, mlolongo wa kutoa au kuhamisha fedha ndiyo usalama wako.
Kuwa makini na watu usiowajua
Unaweza kukutana na mtu mgeni anayeonekana kutaka kukuzoea ghafla. Anaweza kuwa anakufahamu kwa kiasi fulani lakini unapotaka kumjua yeye anakupa hadithi ambazo kila ukijitahidi kuzielewa akili yako inakataa.
Watu hawa ni hatari, wanaweza kuwa ndiyo wezi wenyewe au wamekuja kutafuta uhakika wa taarifa za uhalifu wanaotaka kuutekeleza kwako.
Kama unafanya biashara, mtu anayetaka kukuibia anaweza kuja zaidi ya mara moja. Huwa ni mwenye wasiwasi na anayependa kuuliza maswali mengi.
Epuka kuzungumzia mipango yako
Unapokaa na watu iwe kazini, sehemu za starehe au mkusanyiko wa aina yoyote usizungumzie mipango yako hasa ile inayohusiana na fedha.
Unapozungumza na simu kuhusu mipango ya fedha hakikisha hakuna anayekusikiliza kwani anaweza kutoa taarifa hizo kwa wahalifu nao wakapanga mbinu ya kukupora au kukudhuru.
Kuwa makini unapotumia mashine za ATM
Usimwamini mtu hasa unapoingia katika mashine za kutolea fedha. Angalia watu waliotangulia au waliopo karibu na eneo la mashine hiyo.
Baada ya kutoa fedha kuwa makini. Ukimuona mtu unayemtilia shaka, badilisha uelekeo. Kama yupo nyuma au mbele yako, vuka upande wa pili wa barabara na ondoka haraka.
Kwa wenye vibanda vya miamala ya fedha:
Wafanyabiashara wa miamala ya fedha ni waathirika wa uporaji kwa kuwa wanaaminika kuwa na fedha wakati wote. Mbinu ya kuepuka kuporwa ni kufunga mapema maduka au vibanda vyao.
Njia nyingine ni kuwa makini na watu wanaofika kuulizia kama wana kiasi fulani cha fedha wakijifanya wanataka kutoa lakini huondoka bila kufanya hivyo.
Hawa ni wahalifu ambao hujihakikishia kwanza kama mlengwa ana fedha za kutosha kabla hawajamvamia kwa hiyo, anapotokea mtu kama huyu ni vyema kumfuatilia na ikibidi kufunga kibanda kabla hajarudi na wenzake kufanya uhalifu.
Kadhalika, ikiwa umekusanya kiwango kikubwa cha fedha, hakikisha unazihamisha na kubaki na kiasi ambacho kitahitajika kwa miamala katika muda wa kazi uliobaki.
Post a Comment
Post a Comment