WINGU zito vilio majonzi na simanzi vilitanda kutokana na vifo vya watoto wawili wa maofisa wa Jeshi la Magereza waliofariki dunia kwa kukosa hewa baada ya kujifungia kwenye gari la mmoja wa wazazi wao walimokuwa wakicheza.
Tukio hilo limetokea juzi jioni katika Kota za Magereza Ukonga jijini Dar es Salaam, wakati wazazi wao walipokuwa wakitengeneza gari hilo lililogoma kuwaka.
Watoto waliopoteza maisha ni mtoto wa Mrakibu wa Jeshi la Magereza (ASP), Demetrus Masala, aitwaye Maria (6), ambaye alikuwa darasa la kwanza katika Shule ya Mtakatifu Therese Ukonga na Sajini Francis, ambaye ni Esther (4), mwanafunzi wa shule ya awali katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo ambao hawakupenda majina yao yaandikwe kwenye vyombo vya habari kwa sababu si wasemaji wa familia walidai kuwa watoto hao walipoteza maisha katika gari lenye namba ya usajili T 291 CXR aina ya Toyota Passo ,mali ya ASP Masala.
Mashuhuda hao walidai kuwa siku ya tukio gari hilo liligoma kuwaka na ndipo Masala alipokwenda kumuomba jirani yake ambaye anaishi mlango wa pili Sajini Francis aende kumsaidia kulibusti ambapo alichukua betri katika gari yake ili amsaidie jirani yake huyo.
Ilielezwa kuwa licha ya kuibusti betri ya gari la ASP Masala haikupokea moto ikiashiria kuwa Alternator ilikuwa ni mbovu kwani ilikuwa haifui umeme.
Baada ya kushindikana kuiwasha gari hilo waliamua kuachana nalo na kushauriana ASP Masala aende kumfuata fundi na ndipo alipolifunga gari lake na kuondoka pasipo kujua watoto wao walikuwa ndani ya gari hilo kwani walipokuwa wakilitengeneza walionekana wakiwa pembeni yake.
Post a Comment
Post a Comment