Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein ametangaza neema mpya kwa wafanyakazi visiwani humo baada ya kuwakikishia kupandisha kima cha chini cha mshahara kuanzia mwaka huu (2017).
Dkt. Shein ametoa hakikisho hilo jana wakati akiwaongoza watanzania kuadhimisha Miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar katika sherehe zilizofanyika katika uwanja wa Amani visiwani humo.
Alisema kuanzia mwaka huu kima cha chini cha mshahara kitaongezeka kutoka Tsh. 150,000 hadi Tsh. 300,000 ikiwa ni ongezeko la asilimia 100.
Dkt. Shein alitoa tathmini yake ya mwaka mmoja tangu achanguliwe tena kuiongoza Zanzibar, ambapo alisema mwaka 2016 umekuwa ni wa mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu, kilimo, viwanda, huduma za jamii ikiwemo afya na huduma za maji, miundombinu n.k.
Akihutubia kwenye uwanja wa Amani Dkt. Shein alisema, serikali yake itaendelea kudumisha na kuenzi umoja na mshikamano ambao uliasisiwa na viongozi wa mapinduzi hayo.
Alisema, mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kukuza pato la taifa hadi kufikia 6.6% licha ya kuongezeka kwa mfumuko wa bei kutoka 5.7% katika mwaka 2015 hadi kufikia 6.7% mwaka 2016.
Pia Dkt. Shein alieleza utekelezaji wa sera ya kulipa pensheni kwa wazee, ambapo amesema hadi mwezi Desemba mwaka 2016, jumla ya shilingi bilioni 4.3 zimetumika kuwalipa wazee 25,259 waliosajiliwa kiasi cha shilingi 20,000 kila mwezi, zoezi ambalo litaendelea kutekelezwa.
Katika hatua nyingine, Dkt Shein alitangaza rasmi kuwa matangazo yote ya TV yatahama kutoka mfumo wa 'Analogue' na kuhamia mfumo wa 'kidigitali' kuanzia mwezi April mwaka huu.
Post a Comment
Post a Comment