Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara imeiamuru kampuni ya Uingereza yenye makao yake Kenya, British American Tobacco Kenya Limited (BAT), kuilipa fidia ya Sh6.2 bilioni kampuni ya Mohan’s Oysterbay Drinks Limited ya nchini.
Uamuzi huo unatokana na Mahakama kuridhika kuwa kulikuwa na makubaliano ya kibiashara kati ya Mohan’s na BAT ambayo iliyavunja.
Mohan’s iliomba kulipwa Sh12 bilioni zikiwa ni fidia ya uwekezaji iliofanya kutokana na makubaliano hayo, hasara ya kibiashara, faida waliyoitarajia, hasara ya jumla na riba. Makubaliano hayo yalihusu usambazaji wa sigara zinazozalishwa na BAT aina ya Dunhill na Benson & Hedges.
BAT ilikana kuwa na uhusiano wa kibiashara na Mohan’s kama msambazaji wa bidhaa zake kwa madai kuwa hapakuwa na mkataba wa maandishi, bali uhusianao wao ulikuwa ni muuzaji na mnunuzi.
Jaji Latifa Mansoor katika hukumu ya kesi hiyo, amesema vielelezo vilivyowasilishwa na Mohan’s mahakamani vinabainisha kulikuwa na makubaliano ya kibiashara ya mtengenezaji na msambazaji na si muuzaji na mnunuzi.
Amesema BAT haikuwa na sababu ya msingi kuvunja makubaliano kwa kuwa haikuonyesha kuwa Mohan’s ilitenda kosa la ukiukaji wa makubaliano lililosababisha kuyasitisha baada ya kuwapo uhusiano wa kibiashara wa miaka 19.
Jaji Mansoor amesema BAT ingeweza kujadiliana na Mohan’s kuhusu masharti yenye manufaa kwa makubaliano ya usambaji bidhaa hizo, huku wakiweka kifungu cha kuyasitisha jambo ambalo lingewezesha kuendeleza biashara kwa muda mrefu.
Licha ya kukubaliana na madai ya Mohan’s kuhusu uhusiano wake na BAT, hata hivyo Jaji Mansoor hakukubaliana na kiwango cha fidia ambacho kampuni hiyo ya Mohan’s ilikuwa imekiomba cha Sh12,079,000,000.
Badala yake Jaji Mansoor ameamuru kampuni hiyo ya BAT kuilipa Mohan’s fidia ya jumla ya Sh6,234,835,855 (zaidi ya Sh6.2 bilioni), ikiwa ni fidia ya hasara ya gharama za uwekezaji, hasara ya kibiashara, hasara ya jumla,
Pia ameiamuru BAT kulipa asilimia 12 ya kiasi hicho tangu siku ya hukumu hadi itakapokamilisha malipo hayo na pia kulipa gharama zote za kesi hiyo.
Jaji amesema katika hukumu hiyo kuwa kampuni hiyo imeshindwa kuthibitisha madai mengine kiasi cha Sh12 bilioni ilichokuwa ikiomba, kama vile mapato ya mauzo waliyokuwa wakiyatarajia, malipo ya fidia na malipo ya bima kwa wafanyakazi waliowapunguza.
Mohan’s kupitia kwa Wakili wake Dillip Kesaria ililieleza Mwananchi kuwa ingawa madai yake ya fidia ya zaidi ya Sh12 bilioni iliyokuwa ikiiomba hayakukubaliwa, lakini wameridhika na hukumu hiyo na kiasi cha zaidi ya Sh6.2 bilioni walizopewa na Mahakama.
Wakati Mohan’s ikieelezea kuridhika na hukumu hiyo, BAT kwa upande wake kupitia kwa Wakili wake, Karume, ililieleza kuwa haikuridhika na hukumu hiyo na kwamba itakata rufaa katika Mahakama ya Rufani kuipinga.
Wakili Karume alibainisha kuwa tayari wameshachukua hatua za awali za kukata rufaa kuipinga hukumu hiyo, kwa kuwasilisha mahakamani taarifa ya kusudio la kukata rufaa.
“Hivyo kwa sasa tunasubiri tu kupata mwenendo wa kesi hiyo ili tuweze kukata rufaa rasmi kwa kuwasilisha mahakamani sababu za rufaa yetu,”amesema Wakili Karume.
Post a Comment
Post a Comment