BAADA ya kuwa nje ya ulingo wa siasa takribani mwaka mmoja, hatimaye mbunge wa zamani wa Nyamagana, Ezekiel Wenje amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Kanda ya Ziwa Victoria.
Wenje alitangazwa juzi kupitia uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema kuwa mgombea uenyekiti wa chama hicho kabla ya kuibuka mshindi katika uchaguzi uliojumuisha wagombea kutoka mikoa ya Geita, Mwanza na Kagera yenye majimbo ya uchaguzi 25.
Mbunge huyo wa zamani alikuwa akichuana na Meya wa Manispaa ya Bukoba Mjini, Chifu Kalumuna ambapo katika uchaguzi huo uliofanyika juzi saa tatu usiku, Wenje aliibuka mshindi.
Hadi juzi jioni wagombea wanne ndio waliotajwa kuwania nafasi hiyo, akiwamo aliyewahi kuwa Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima, Ansbert Ngurumo, ambaye katika uchaguzi huo alihamishiwa kugombea nafasi ya Umakamu Mwenyekiti na kuibuka mshindi.
Awali, wagombea wengine wa nafasi hiyo akiwamo aliyekuwa Mwenyekiti wa Kanda hiyo, Peter Makere na Ofisa wa Chama hicho, Tungaraza Njugu waliondolewa kuwania nafasi hiyo.
Akizungumzia kuchaguliwa kwake kushika nafasi hiyo, Wenje alisema: “Nitafanya kazi kwa kushirikina na viongozi wenzangu kuhakikisha tunaijenga Kanda ya Ziwa. Tutahakikisha tunashinda katika uchaguzi ulio mbele yetu, kasi yangu niliyokuwa nayo nitaendelea nayo hiyo hiyo.”
Itakumbukwa kuwa katika uchaguzi wa mwaka jana, Wenje aliyekuwa na nguvu katika jimbo la Nyamagana aliangushwa na Stanslaus Mabulab wa CCM.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Viti Maalumu Mwanza, Suzan Masele aliyekuwa akigombea nafasi ya uhazini aliangusha na Bugomba Mzuba.
Post a Comment
Post a Comment