MWANZA: MTOTO ALIWA NA FISI AKISUBIRI CHAKULA CHA USIKU

Tarehe 24.07.2017 majira ya saa 11:00 alfajiri katika Mtaa wa Kabangaja Kata ya Bugogwa Wilaya ya Ilemela jiji na Mkoa wa Mwanza, makusudi Rashidi miaka 39, mkazi wa Mtaa wa Ibangaja, anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kumbaka binti wa miaka 11 (jina tunalihifadhi) na kumsababishia maumivu makali sehemu zake za siri, kitendo ambacho ni kosa la jinai.

Awali inadaiwa kuwa, alfajiri ya majira tajwa hapo juu wazazi wa majeruhi aliyebakwa waliondoka na kwenda kutafuta riziki ya watoto huku nyumbani wakiwaacha majeruhi na mdogo wake wakiwa wamelala. Inasemekana kuwa wakati majeruhi akiwa amelala na mdogo wake, ghafla alishtuka na kumuona mtuhumiwa tajwa hapo juu akiwa anambaka kwa nguvu huku akisikia maumivu makali na kupelekea kupiga kelele za yowe akiomba msaada, inadaiwa kuwa baada ya mtuhumiwa kuona hali hiyo alitoka nje na kuanza kukimbia.

Wananchi walifika kwa haraka eneo la tukio kutoa msaada ambapo baada ya kufika walimuona mtuhumiwa akiwa anakimbia na kuanza kukimbiza hadi walifanikiwa kumkamata kisha wakatoa taarifa kituo cha polisi, askari walifanya ufuatiliaji wa haraka juu ya taarifa hizo hadi eneo la tukio na kumkuta mtuhumiwa akiwa chini ya ulinzi wa wananchi.

Polisi wapo katika mahojiano na mtuhumiwa pindi uchunguzi ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani, majeruhi tayari amepelekwa hospitali kupatiwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishina wa Polisi, Ahmed Msangi ametoa wito kwa wakazi wa jiji na mkoa wa mwanza hususani wazazi/walezi akiwaomba kuwa na makazi salama yatakayoweza kuwalinda watoto na mali dhidi ya wahalifu. Aidha pia amewataka wananchi wa Mwanza kuwa waangalifu na makini wakati wote na watu wenye nia ovu dhidi ya watoto.

Katika tukio la pili;

Mnamo tarehe 23.07.2017 majira ya 9:00 jioni katika Kitongoji cha Izizimba, Kijiji cha Izizimba “A” Kata ya Mhande, Tarafa ya Mwamashimba, Wilaya ya Kwimba, Mkoa wa Mwanza, mtoto wa kike aliyefahamika kwa jina la Limi Bunzama, miaka 04, mkazi wa Kijiji cha Izizimba “A”, amefariki dunia baada ya kukamatwa na fisi wakati akiwa anacheza na baadae kuliwa sehemu mbalimbali za mwili wake hadi kufariki dunia.

Inadaiwa kuwa marehemu alikuwa na mama yake nje ya nyumba yao akiwa anacheza huku wakiwa wanasubiri chakula cha usiku. Inasemekana kuwa wakati marehemu akiwa anacheza mbali kigodo na alipo mama yake ghafla alifika mnyama fisi na kumkamata kisha kukimbia nae vichakani. Mama wa marehemu alisikia kelele za mtoto wake akilia ndipo alianza kumfuatilia huku akipiga yowe akiomba msaada.

Inasemekana kuwa majirani walifika eneo la tukio na kushirikiana na wazazi wa marehemu kumfuatilia fisi huyo, lakini kwa bahati mbaya walichelewa kwani walikuta tayari fisi amemuua mtoto na kumla sehemu mbalimbali za mwili wake kisha kukimbia kichakani. Aidha mabaki ya mwili wa marehemu tayari yamefanyiwa uchunguzi na daktari na kukabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi. Chanzo cha kifo hicho ni uzembe wa wazazi kutokuwa makini na motto.

Juhudi za kumtafuta fisi huyo ili asiendelee kuleta madhara kwa watu na watoto kwa kushirikiana na wananchi bado zinaendelea.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishina wa Polisi, Ahmed Msangi ametoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Mwanza hususani wazazi na walezi akiwataka kuwa waangalifu na makini wakati wote na watoto, ili kuwaepusha na ajali au na vifo vinavyoweza kuepukika.

Imetolewa na:

DCP: Ahmed Msangi

Kamanda wa Polisi (M) Mwanza

Related Posts

Post a Comment