Na John Walter-Babati
Mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange amewaagiza wasimamizi wa miradi katika kata za Halmshauri ya mji wa Babati, kukamilisha miradi ya maendeleo iliyopo katika maeneo yao.
Twange ametoa agizo hilo leo Januari 17, 2024 alipofanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika kata za Bonga, Babati mjini, Bagara na Mutuka huku akiwataka kutenga miradi michache watakayoweza kuimaliza kuliko kuwa na mingi isiyokamilika.
Mkuu wa wilaya amesema Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi kwenye maeneo mengi hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha inakamilishwa kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa na kwa thamani halisi na si vinginevyo.
Katika ziara hiyo, Twange ametaka kujiridhisha na matumizi ya fedha kutoka Halmashauri pamoja na Serikali Kuu namna zilivyotumika kwenye miradi husika, huku akitoa maagizo ya kukamilika mingine ambayo bado.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji wa Babati Pendo Mangali ameahidi kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na mkuu wa wilaya ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika na kutumikas kwa manufaa ya wananchi.
Diwani wa kata ya Mutuka Yona Wawo amesema hatua iliyochukuliwa na mkuu wa wilaya kutembea katika kata na kupata taarifa juu ya miradi ya maendeleo inaongeza kasi ya uwajibikaji na ufanisi katika miradi husika.
Post a Comment
Post a Comment