Timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imeshindwa kupata ushindi kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Lesotho kuwania kufuzu kucheza fainali za mataifa ya Afrika mwaka 2019.
Stars ilitangulia kupata goli la kuongoza dakika ya 27 kipindi cha kwanza likifungwa na mshambuliaji tegemeo Mbwana Samatta kwa mpira wa adhabu ndogo baada ya beki wa kushoto Gadiel Michael kufanyiwa madhambi nje kidogo ya eneo la penati box.
Samatta alipiga mkwaju wa moja kwa moja uliomshinda golikipa wa Lesotho Likano Mphuti na kujaa nyavuni kulia kwa golikipa huyo.
Haikuchukua dakika nyingi, Lesotho wakasawazisha bao hilo dakika ya 36 kipindi cha kwanza baada ya uzembe wa safu ya ulinzi wa Stars na kutoa nafasi kwa Likano Mphuti kufunga bao.
Lesotho baada ya kupata bao walianza kucheza kwa tahadhari, wakijilinda na kupoteza muda kulinda matokeo ya sare ya 1-1 na kuambulia pointi moja ugenini.
Matokeo hayo yamedumu hadi dakika 90 zinamalizika na Stars imeambulia pointi moja kwenye mchezo huo.
Kikosi cha Stars kiliongozwa na Aishi Manula, Shomari Kapombe, Gadiel Michael, Abdi Banda, Salim Mbonde, Himid Mao, Simon Msuva/Farid Musa Mzamiru Yassin/Salum Abubaka, Thomas Ulimwengu/Mbaraka Yusuph, Mbwana Samatta na Shiza Kichuya.
Wachezaji wa benchi ambao hawakutumika: Said Mohamed, Hassan Ramadhani Kessy, Erasto Nyoni na Nurdin Chona.
Post a Comment
Post a Comment