Baada ya kupoteza mechi iliyopita, timu ya Mtanzania Thomas Ulimwengu leo Jumamosi itakuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Tunavallen kucheza na Oerebro katika muendelezo wa Ligi Kuu ya Sweden.
Katika mchezo uliopita, Eskilstuna ilifungwa mabao 3-1 na GIF Sundsvall hali iliyowafanya kushika nafasi ya 14 katika msimamo wa timu 16 za ligi hiyo. Hata hivyo hii ni mechi ya pili ya ligi hiyo.
Kocha wa Eskilstuna, Pelle Olsson leo atakuwa na chaguo la kumtumia Ulimwengu au la baada ya mshambuliaji huyo kupona majeraha ya kifundo cha mguu yaliyokuwa yakimuanda kwa muda mrefu.
Hata hivyo, itategemea na ripoti ya daktari na jinsi Ulimwengu alivyo tayari kulingana na mazoezi aliyofanya mapema wiki hii na kikosi cha kwanza baada ya kupona.
Kama mambo yataenda vizuri, straika huyo atakuwa ameianza safari yake ya kuitumikia timu yake hiyo aliyojiunga nayo hivi karibuni baada ya kumaliza mkataba na TP Mazembe ya DR Congo.
Meneja wa Ulimwengu, Jamal Kisongo hivi karibuni alisema Ulimwengu kwa sasa yupo tayari kwa mapambano baada ya kupatiwa matibabu maaalum kutibu majeraha yake.
“Nimewasiliana na Ulimwengu ameniambia ameshapona na yupo tayari kwa mapambano kuhakikisha anapata nafasi kwenye kikosi cha kwanza,” alisema Kisongo.
Post a Comment
Post a Comment