Mshambuliaji wa klabu ya Manchester United Zlatan Ibrahimovic anaamini ameliteka soka la Uingereza ndani ya kipindi cha miezi mitatu tangu alipo jiunga na United.
Amesema hana malengo binafsi yaliyobakia kwake badala yake ameelekeza nguvu na akili zake kushinda ubingwa wa Ligi Kuu Uingereza.
Ibrahimovic ambaye anaumri wa miaka, 35, amekuwa na ushawishi mkubwa tangu alipotua Uingereza akitokea Paris Saint-Germain kwa uhamisho huru, magoli yake 13 ya ligi yakimwacha nyuma ya Diego Costa wa Chelsea katika mbio za kuwania kiatu cha dhahabu.
Lakini Ibrahimovic amesisitiza kuwa lengo lake kuu ni kuisaidia United kuendeleza mwendo wao wa ushindi wa mechi tisa katika michuano yote, ligi ikiwa kipaumbele chake kikuu.
Mshambuliaji huyo aliuambia mtandao wa United: “La! Sifukuzii mtu yeyote. Nafukuzia taji kuu – Ligi Kuu.
“Hilo ndilo dhumuni langu. Mafanikio binafsi huja kama sehemu ya malengo makuu kwa sababu hayo ni kama bonasi kwa kila mchezaji binafsi.
“Sina malengo binafsi kwa sababu nimeshayafanya, baada ya miezi mitatu katika Uingereza. Imenichukua miezi mitatu kuiteka Uingereza.
“Ikiwa kwa pamoja tunafanya vizuri, kila mtu atafanya vizuri binafsi. Najaribu kuisaidia timu na ninajaribu kufanya kile ninachokimudu zaidi – kufunga magoli, kucheza vizuri na kutengeneza nafasi kwa ajili ya wachezaji wenzangu.
United inakabiliwa na mtihani mkubwa katika mechi yao ya Jumapili dhidi ya Liverpool, na Ibrahimovic ameweka bayana kuwa lengo lao kuu ni kupunguza pengo la pointi dhidi ya timu hiyo ya Jurgen Klopp.
“Mwezi mmoja na nusu uliopita umejidhihirisha wenyewe, pengo lilikuwa kubwa lakini sasa hali ni nzuri,” alisema.
“Tutawapa kazi kubwa sana kwa sababu nadhani duru la pili la msimu ndilo gumu zaidi. Najua tunachokitaka.
“Tuna mabonde na milima yetu tunaposhinda na kushindwa. Hivi karibuni tumekuwa tukishinda tumekuwa timu thabiti zaidi.
“Kocha amepata kanuni nzuri, ambayo si rahisi unapokuja kama kocha mpya kwenye timu mpya na unataka kutumia falsafa yako, na aina ya uchezaji unaoutaka.
“Nilisema hapo mwanzo – pole pole, tutaimarika na mambo yamekuwa.”
Post a Comment
Post a Comment