Siku za mwanamke kupata mimba.

Njia ya kalenda ni moja ya njia ambazo wenye kushikilia mila na desturi na imani za kidini hupendelea kuitumia njia hii ya asili ili kufanya uzazi wa mpango.

Njia ya kalenda ni njia inayohitaji nidhamu kwa wenza wawili na pia inahitaji kujifunza na kuizoea angalau kuifanyia mazoezi kwa muda wa miezi 3-6 vinginevyo njia za vidonge, vipandikizi na sindano ndio zinafanikiwa kukukinga usipate ujauzito.
Wapo waliokuwa wanadhani ujauzito unaweza kupata siku inayofuata baada damu ya hedhi kukata, mwingine alikuwa akijua kuwa kuifahamu siku ya hatari ambayo yai limekomaa tayari zinahesabiwa kutoka mara ya mwisho damu ya hedhi kuisha.

Kawaida wanawake walio wengi duniani kwa mujibu wa machapisho mbalimbali ya kitafiti ya kisayansi mzunguko wa hedhi wa kawaida ni siku 28-30 karibu asilimia 85-90. Ingawa wapo wachache ambao wana mzunguko mfupi wa siku 21 na wapo wenye mzunguko wa mrefu wa hedhi wa siku 35-42.

Mwanamke hupata hedhi kipindi ambacho kama mimba haikutungwa ngozi nyororo iliyomo katika mfuko wa uzazi hunyofoka na kutolewa nje kama damu ya hedhi. Katika mzunguko wa hedhi kipo kipindi maalumu ambacho kiyai cha kike huwa tayari kimekomaa na endapo kitakutana na mbegu ya kiume mimba huweza kutungwa.

Kipindi hiki huwa ni siku ya 14 kwa wanawake walio wengi ambao mzunguko wao ni siku 28, huhesabiwa tangu siku ya kwanza lilipotoka tone la damu ya hedhi na sio siku ya mwisho hedhi ilipokata.

Ili kuweza kujua siku za kupata mimba inakubidi kuhesabu siku ya kwanza kupata hedhi mpaka siku ya 14 kwa wale wanawake wenye mzunguko siku 28.

Kwa kawaida wanawake wote hata kama wana mizunguko ya hedhi ina urefu wa siku isiyo sawa zile siku za matayarisho yai kutengenezwa huwa ni sawa ambazo huwa ni siku 14. Ili kuweza kujua siku yako ya kupata mimba unachukua siku 14 unatoa kwa siku za mzunguko wako. Kwa mfano, kama wewe uliyeuliza swali mzunguko wako ni siku 30 unatoa kwa 14, hivyo unapata 16.

Hivyo yai lako linakuwa limekomaa na kuweza kurutubishwa na mbegu ya kiume katika siku ya 16. Nitoe mfano mwingine; tuchukulie una mzunguko wa mfupi ambao ni siku 21 ili kujua siku yako hasa ya yai kuwa limekomaa unatoa siku 14 hivyo unapata 7.

Mtu mwenye mzunguko wa siku 21 yai lake linakuwa limekomaa siku ya 7. Kwa wenye mzunguko wa siku 28 ambao ndiyo wengi unachukua 14 unatoa 28 unapata siku 14. Ndiyo maana inazungumzwa kuwa siku ya 14 ndiyo siku ya hatari kwa wanawake wengi ndio maana wanaiepuka bila kujua pia mwenye mzunguko wa siku 28 pia ana nafasi ya kupata katika siku ya 11, 12, 13, 15, 16, 17 na 18.

Hivyo basi ili kuweza kuondoa uwezekano wa kupata mimba unaweza kutumia kanuni ya kujumlisha siku 3 au kutoa 3 pale unapojua siku yako ya hatari. Ingawa wengine huamua kutumia kujumlisha au kutoa 4.

Kwa yule aliyeuliza swali ambaye ana mzunguko wa siku 30, ambaye tumejua kuwa siku yake yai kuwa limekomaa tayari ni siku ya 16. Hivyo tukijumlisha siku 3 tunapata siku 17, 18, 19 wakati tunapotoa siku 3 tunapata siku ya 15, 14, 13.

Hivyo basi siku zako za hatari ambazo unaweza kujikuta unapofanya tendo bila kinga yoyote ya uzazi wa mpango unaweza kupata mimba ni siku ya 13-19 (Kwa mwenye mzunguko wa siku 30).

Ingawa ni kweli kuwa siku ya kuweza kupata mimba hasa ni moja lakini zipo siku ambazo pia zinakuwa na nafasi ya kuweza kupata mimba, ambazo huwa tunaziita siku za hatari kitabibu huitwa unsafe days.

Kwa kuwa yai la kike huwa na uwezo wa kurutubishwa na kuwapo kwa muda wa saa 24-78, mbegu za kiume huwa na uwezo wa kuwa hai kwa saa 24-48.

Hivyo basi kama utakutana na mwenza wako siku ya 11, 13 au 15, 16 unaweza kupata mimba. Kwa mfano, kama utakutana na mwenza siku ya 16 na yai la kike likiwa limekomaa siku ya 14 kuna nafasi ya kupata ujauzito kwa sababu kiyai cha kike linaweza kuwa hai kwa siku moja mpaka tatu.

Vilevile kama utakutana na mwenza wako siku ya 12 wakati kiyai cha kike bado siku mbili kukomaa, nafasi ya kupata mimba ni kubwa kwa sababu mbegu ya kiume huwa na uwezo wa kuwa hai kwa siku mbili, hivyo itakapokutana na yai siku ya 14 mimba hutungwa.

Zipo dalili ambazo hujitokeza ambazo huashiria kuwa yai la kike huwa tayari limekomaa na mimba kuweza kutungwa. Dalili ni kama vile ute wa uke huwa mzito na mwingi ukilinganisha ni siku za kawaida.

Endapo utavuta na kidole gumba na kidole cha shahada huwa ute huo haukatiki, ute huo huwa na rangi kwa mbali kama vile kutu. Joto la mwili huwa juu. Matiti na upande wa kulia chini ya tumbo huuma kwa mbali, kujihisi hamu ya kufanya tendo la ndoa, pia kuna uthibitisho kuwapo kwa harufu fulani maalumu ambayo humpa msisimko mwanaume.

Related Posts

Post a Comment