NJIA RAHISI ZA KUONDOA HARUFU MBAYA MWILINI

Kila mtu ana jasho au harufu ya kipekee mwilini na ndiyo maana kila mtu ana mahitaji ya kipekee katika kutunza mwili wake. Viungo vifuatavyo ndivyo hasa vinavyotoa harufu mbaya:

KINYWA

Kuna wakati kinywa hutoa harufu mbaya isiyovumilika. Wapo ambao hata wakipiga mswaki kwa kutumia dawa ya meno mara hata 100 harufu hubaki pale pale. 
Tatizo hili husababishwa na matumizi ya mara kwa mara ya kahawa, vyakula vyenye viungo vingi kama pilau, uvutaji wa sigara, pombe au mdomo wa mhusika mwenyewe.
SULUHISHO

Ni vema mtu mwenye tatizo hili akanunua maji ya kusukutua mdomo yajulikanyo kama ‘Hydrogen Peroxide Mouth Wash’, yanayopatikana katika maduka ya dawa kwa bei isiyozidi Sh 1,500 kwa kichupa.

Anachotakiwa mtu kufanya ni kupiga mswaki na kisha ajaze kifuniko cha kichupa hicho na kusukutua kwa kama dakika mbili hivi, kisha ateme. Baada ya hapo anaweza kusukutua kwa maji ya kawaida. 
Hakika hata kama ulikunywa kreti ya bia au kula sufuria zima la vitunguu, harufu ya mdomo wako itabaki nzuri na hutamkwaza mwenzi wako wa yeyote. 

Waweza kusukutua asubuhi na jioni kabla ya kulala. Kutafuna karoti moja baada ya kula pilau au chakula chenye viungo vikali, au limao baada ya kula samaki nayo husaidia iwapo mhusika hana tatizo la vidonda vya tumbo (hasa kwa upande wa kutumia limao).
KWAPA

Kwapa ni moja ya maeneo yanayoleta kadhia kubwa kwa wengi. Harufu inayotoka huitwa kikwapa. Baadhi ya vyanzo vya tatizo hili ni uvivu wa kuoga na kuacha nywele nyingi kwapani, na wakati mwingine hukaa hivyo hadi zinabadilika rangi na kuwa nyeupe au njano na kujisokota kama ‘dreads’.
Jasho lina kawaida ya kukaa kwapani zaidi kuliko sehemu yoyote mwilini. Kama ilivyo kwa mdomo, kuna baadhi ya watu hata waoge vipi, bado hutoa harufu ya kikwapa. Hii humfanya mtu akose raha na asijue la kufanya.

SULUHISHO

Unapokuwa na tatizo hili, ni vema ukaoga kwa sabuni ya magadi kwa sababu zina nguvu ya kukabiliana na tatizo hili. Pili ni vema kila mtu akawa msafi kwa kunyoa nywele za kwapa angalau mara mbili kwa wiki ili kuruhusu sabuni na maji yafike katika ngozi ya sehemu hiyo.
Baada ya kunyoa waweza kupaka mafuta ya nazi ili kuondoa muwasho. Zaidi ya hapo ni vema tukatumia ‘deodorant’ – manukato ya wanaume au yoyote yale yenye harufu nzuri kwa jinsia. Wapo pia kina mama wanaonuka kikwapa. 

Usisahau pia kuoga kabla ya kulala. Waweza pia kutumia manukato yasiyo makali au ‘body spray’ zenye harufu nzuri kiasi kutokana na uwezo wako, ili kukufanya unukie vizuri.
SEHEMU ZA SIRI 

Nadhani wengi tunaelewa maana yake. Tatizo hili pia hukera na kumkosesha raha mlengwa. Sababu kubwa za kutoa harufu ni pamoja na kutooshwa au kusafishwa mara kwa mara hasa – mtu anapomaliza haja zake za namna yoyote. Pia kutobadili nguo za ndani mara kwa mara.

SULUHISHO 

Kwanza hatuna budi kuwa na tabia ya usafi kwa kuoga walau mara mbili kwa siku. Kunyoa sehemu hizo pia walau mara mbili kwa wiki. Kina mama nao wawe makini zaidi wakati wa siku zao, kwa kuoga na ‘kuvaa nguo maalumu’ kwa sehemu hizo.
Vilevile, tusianike ndani au kuvaa nguo zenye unyevunyevu, kwani huleta fangasi. Kama umeshindwa kuanika nje, basi piga pasi kabla ya kuvaa. Sehemu za siri ndio kama Ikulu yetu.
La mwisho kwa kina mama, ni vema tukafanya usafi mara moja baada ya ‘sakramenti’ na vivyo hivyo kwa wenzi wetu ili harufu ya chumba iwe nzuri. Tusisahau matandiko ambayo nayo ni vema yakawa safi. Pia nawa vema na maji au tumia karatasi ya chooni mara umalizapo kujisaidia.
MIGUU 

Miguu nayo hutoa harufu wakati mwingine, hasa kwa kina baba wanaovaa viatu na soksi – iwe wakati wa joto au mwingine wowote. Tatizo hilo huweza pia kuwakumba hata kina mama.

SULUHISHO 

Kila mtu anaoga. Lakini ni rahisi kuoga na kusahau kuosha kikamilifu miguu na nyayo. Hakikisha unaosha miguu yako asubuhi na jioni. Kausha miguu hasa katikati ya vidole na kisha nyunyuzia poda maalumu inayoitwa ‘Cotrimazole’ na pia kwenye soksi.

Poda hii inapatikana katika maduka ya dawa kwa kati ya Sh 3,500 na Sh 4,000. Kuna poda nyingine inaitwa Mycota, waweza pia kununua na kutumia japo bei yake ipo juu kidogo. 
NYWELE

Nimalizie kwa kuzungumzia nywele hasa kwa kima mama. Ni vema wakaosha nywele zao angalu mara moja kwa wiki – wana matengenezo yao ya nywele, hilo tutalizungumzia siku yake maalumu – na kuvaa kofia ya wavu wakati wa kulala ili zisitoe jasho sana kwani nayo ni kadhia kubwa.

Related Posts

Post a Comment