SERIKALI KUPIGA MNADA MALI ZA WADAIWA SUGU

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angeline Mabulla ameziagiza halmashauri zote kuwafikisha mahakani na kuuza mali zao wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi wenye madeni ya muda mrefu.



Dkt. Mabulla ametoa agizo hilo wakati alipofanya ziara ya kukagua mifumo ya makusanyo ya kodi ya ardhi mkoani Geita mara baada ya kukuta majina 100 ya wadaiwa wa kodi ya ardhi ambao hawajalipa kwa zaidi ya miaka 10.

Mhe. Naibu Waziri wa Ardhi alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Geita kuhakikisha wadaiwa hao wa muda mrefu wanaandikiwa notisi ya muda wa siku 14 na wasipolipa ndani ya muda huo wafikishwe mahakamani bila kuchelewa na kama wasipolipa basi mali zao zipigwe mnada.

Mara baada ya kubaini hayo Mhe. Mabulla amefanya upekuzi wa nyaraka za umiliki wa ardhi katika masijala ya ardhi ya Halmashauri ya mji wa Geita na kugundua uhifadhi mbovu wa hati na ucheleweshwaji utoaji hati za wamiliki kwa muda mrefu.

Naibu waziri alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Geita kutembelea mara kwa mara katika ofisi na masijala za ardhi ili kuhakikisha maafisa wa idara ya ardhi wanatoa hati kwa wakati na kwa mpangilio mzuri bila kuleta migogoro.

Aidha, Naibu Waziri huyo alitembelea eneo lenye viwanja vilivyowekwa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita ambavyo vimepangwa kujengwa ofisi za serikali, shule, hospitali, makazi, maeneo ya kuzikia, na huduma nyingine za kijamii.

Naibu Waziri alimtaka mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale kihakikisha mji huo unapangwa vizuri na kuwekwa miundombinu ya barabara, maji safi na taka na umeme ili kuepusha migogoro ya ardhi ambayo mara nyingi huibuka kutokana na wilaya kutokuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi ya muda mrefu.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angeline Mabulla ametembelea eneo la Bombambili mkoani Geita lililojengwa nyumba 48 za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambapo nyumba 14 tayari zimenunuliwa na Halmashauri ya mji wa Geita.

Mhe. Mabulla alizitaka halmashauri nyingine nchini kuiga mfano wa halmashauri ya mji wa Geita kwa kuwashirikisha NHC katika kujenga nyumba bora badala ya kutumia wakandarasi wa nje wakati Shirika la Nyumba la Taifa lipo na linajenga nzuri na kwa gharama nafuu.

Naye Meneja wa NHC Mikoa ya Mwanza, Geita na Simiyu Eng. Benedict Kilimba alimeishukuru Halmashauri ya mji wa Geita kwa kuwa wakwanza kununua nyumba hizo 14 katika hatua ya awali.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angeline Mabulla anaendelea na ziara yake ya mikoa ya kanda ya ziwa ambapo anataria kufanya ziara Mkoa wa Shinyanga hasa katika wilaya ya Kahama na Shinyanga Mjini.



Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angeline Mabulla akihakiki amefanya upekuzi wa nyaraka za umiliki wa ardhi katika masijala ya ardhi ya Halmashauri ya mji wa Geita, kushoto ni Kaimu Kamishna wa Ardhi Msaidizi Kanda ya Ziwa Bw. Makwasa Biswalo na katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Geita Bw. Herman Kapufi.



Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angeline Mabulla akikagua nyumba 48 zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) eneo la Bombambili mkoani Geita kushoto ni Meneja wa NHC Mikoa ya Mwanza, Geita na Simiyu Eng. Benedict Kilimba.



Naibu Waziri wa Ardhi, Mhe. Dkt. Angeline Mabulla akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Geita Bw. Herman Kapufi (kulia) na Meneja wa NHC Mikoa ya Mwanza, Geita na Simiyu Eng. Benedict Kilimba (kushoto) wakikagua nyumba 48 zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) eneo la Bombambili mkoani Geita.



Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angeline Mabulla akihakiki majalada ya wamiliki wa ardhi katika masijala ya ardhi ya Halmashauri ya mji wa Geita.

Related Posts

Post a Comment