KISA CHA NDEGE NDOGO (DRONE) ILIYOPELEKEA MZEE WA GHANA KUHIJI MAKA

Share this
Mzee Al-Hassan Abdullah ni mzee masikini anayeishi kijijini nchini Ghana. Hadithi yake ilisambaa sana kwenye mitandao ya kijamii nchini Uturuki baada ya mzee huyo kuwauliza wafanyakazi wa kituo cha runinga cha nchini Uturuki waliokuwa wakirekodi kipindi nchini Ghana iwapo ndege ndogo isiyokuwa na rubani (drone) iliyokuwa inatumiwa na wafanyakazi hao kurekodi “kama ndege hiyo inaweza kumpeleka Makka kuhiji” amesafirishwa kwenda Mji huo Mtakatifu kwa imani ya Uislam kwa gharama za Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki na michango iliyotolewa na raia mbalimbali nchini Uturuki walioguswa na alichokisema Mzee Abdullah.
Kilichotokea ni kwamba ndege hiyo ilidondoka karibu kabisa na nyumba ya Mzee Abdullah wakati waandishi hao wanarekodi kipindi maalum. Mzee huyu baada ya kuiona ndege hiyo aliiokota na kumsubiri rubani wake aliyekuwa anaifata aichukue. Akiwa anamkabidhi rubani ndege hiyo, ndipo Mzee Abdullah akamuuliza iwapo wana ndege nyingine kubwa zaidi ya hiyo inayoweza kumpeleka mpaka Makka ili akatimize ibada ya kuhiji kama walivyo mamilioni ya waumini wengine watakaohiji mwaka huu. Rubani huyo aliamua kupimga picha mzee huyu na kuandika maneno aliyoulizwa kisha kuituma kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii. Ujumbe huu ulisambaa mara moja na kuwagusa wengi kiasi cha Serikali ya nchi hiyo kuamua kulipia safari yake. Wananchi walioguswa pia waliweza kutoa mchango wao kama sadaka kumuwezesha kwenda kutimiza ibada hiyo.
Ujumbe wake uliposambaa sana kwenye mitandao ya kijamii nchini Uturuki, Waziri wa Nchi za Nje, Mevlüt Çavuşoğlu aliguswa na kushughulikia safari ya mzee Abdullah ambaye ni masikini wa kutupwa kwenda Makka. Mzee Abdullah aliwasili jijini Istanbul, Uturuki juzi Ijumaa akitokea Accra, Ghana na alipokewa na Shirika la Misaada nchini Uturuki ambalo limelenga kusaidi nchi ya Ghana.
Mzee Al-Hassan Abdullah: Kushoto alipokuwa anamkabidhi rubani ndege ndogo baada ya kuanguka karibu na nyumba yake Kulia ni katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa Istanbul, Uturuki
Abdullah aliliambia Shirika la Utangazaji la Anadolu la jijini Ankara, Uturuki kuwa amefurahi kuwa jijini Istanbul na kwamba ni Mungu ndiye aliyembariki kuweza kupata msaada kutoka Serikali ya Uturuki. “Namshukuru Mungu na namuombea kila aliyenisaidia kutimiza ndoto yangu. Msaada wa Serikali ya uturuki ni wa muhimu sana kwangu na ninaamini utakuwa ni uthibitisho wa urafiki kati ya mataifa yetu na kuonesha udugu kwa waislam,” alisema.
Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya misaada iliyompokea mzee huyu, Cihad Gökdemir amesema kwamba ujumbe wa Mzee Abdullah ulisambaa zaidi kwenye vyombo vyote vya habari nchini humo baada ya mfanyakazi wa kituo hicho cha runinga kuweka picha ya mzee huyo kupitia mtandao wa Twitter. “Hapo ndipo watu wengi walipoanza kuwasiliana na mfanyakazi huyo awaongoze jinsi ya kumsaidia Mzee Abdullah, watu wote – wafanyabiashara hadi makampuni. Mwisho, Ofisa wa Polisi kutoka Ubalozi wa Uturuki nchini Ghana akawasiliana naye. Anawashukuru sana watu wa Uturuki,” alisema Gökdemir.

Related Posts

There is no other posts in this category.

Post a Comment