MATONYA KUISHI KENYA BAADA YA KWAHUSISHWA NA DAWA ZA KULEVYA


Msanii wa muziki wa kizazi kipya toka jijini Tanga, Matonya amekimbilia nchini Kenya. Matonya yupo nchini humo kwa muda wa miezi mitatu sasa na inasadikiwa kuwa ana mpango wa kuyafanya kuwa makazi yake ya kudumu.

Baada ya kuhamia huko rasmi, Matonya amekuwa msanii wa pili wa Bongofleva baada ya kufuata nyayo za aliyekuwa msanii mkubwa katika miondoko hiyo, Mr. Nice anayesemekana kuishi maeneo ya Thika.

Tovuti ya TUKO.co.ke imeripoti kuwa mwanamuziki huyo amekuwa nchini Kenya kwa miezi mitatu iliyopita na kwamba amesema kuwa anategemea kuifanya nchi hiyo kuwa makazi yake ya kudumu. Akizungumza na Mzazi Willy M. Tuva, Matonya alikataa madai hayo ya kuhamia nchini Kenya ili akwepe mashtaka yanayomkabili ya kuhusika na madawa ya kulevya nchini Tanzania.

“Sijakimbia Tanzania kwa sababu ulizosema,” amesema Matonya, ambaye Wakenya wengi walimtambua na kumpenda kwa ngoma yake ya Vaileti. “Mliona orodha ya waliosadikiwa kujihusisha na madawa ya kulevya. Jina la Matonya halikuwamo kwenye orodha hiyo. Mimi ni mtu safi na haya mengine unayosikia ni maneno tu yanayosemwa kunichafulia jina.”

Matonya alisema haya alipokuwa kwenye mahojiano na kipindi cha Mambo Mseto cha mtangazaji anayejulikana kwa jina maarufu kama Mzazi wa kituo cha redio cha Citizen na kuongeza kuwa bado yupo nchini Kenya kusimamia miradi yake aliyoianzisha.

Matonya, ambaye tangu aachie ngoma yake ya ‘Nyumba Ndogo,’ amekuwa mwanamuziki wa pili toka Tanzania kuhamia nchini Kenya baada ya Mr. Nice wakati muimbaji wa nyimbo za Injili, Rose Muhando anasemekana pia kuwa yupo kwenye mpango wa kuhamia nchini Kenya.

Related Posts

Post a Comment