WAZIRI Mkuu Ampongeza RC Anna Mghwira Kwa Kuzuia Malori 100 ya Mahindi


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira kwa kuyazuia malori zaidi ya 100 yaliyokuwa yanasafirisha mahindi nje ya nchi.

Jumatatu hii, Majaliwa alipiga marufuku usafirishaji wa mahindi alipokuwa mkoani humo kwa ajili ya sherehe za Sikukuu ya Eid el Fitr.

Baada ya agizo hilo, malori hayo yalikamatwa na kuzuiwa. Akijibu maswali ya papo kwa papo bungeni leo ( Alhamisi) juu ya zuio hilo, Waziri Mkuu amesema uamuzi huo ni moja ya hatua za kuhakikisha Taifa linajihadhari na ukosefu wa chakula hasa ikizingatiwa kwamba kulikuwa na uhaba wa mvua mwaka jana.

"Nampongeza Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro pamoja na kamati yake ya ulinzi na usalama kwa kuyazuia malori hayo," amesema Majaliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana Jumatano, Mghwira alisema magari hayo yalikamatiwa eneo la Himo huku akipiga marufuku usafirishwaji wa nafaka pamoja na sukari kwenda nchi jirani bila ya kuwa na kibali maalumu.

“Baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakisafirisha sukari na nafaka nyakati za usiku huku wakishirikiana na baadhi ya askari polisi ambao si waaminifu, ni vema askari hao wakaacha mara moja kwani ni kinyume cha maadili ya kazi zao,”alisema mkuu huyo wa mkoa.
ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!


Related Posts

Post a Comment