MBOWE ALAANI UDHALILISHAJI WABUNGE WA UPINZANI

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amelaani vitendo vya udhalilishaji na uonevu kwa wabunge wa upinzani vinavyoendelea Bungeni kuwa vinakandamiza Demokrasia na kudhalilisha wabunge wa upinzani. Amedai kuwa baadhi ya matukio na maamuzi Bungeni yamekuwa yakitolewa bila kufuata kanuni na miongozo.

Akitoa kwa mfano wa tukio la kusimamishwa kwa wabunge John Mnyika, Halima Mdee na Esther Bulaya kutohudhuria vikao vya Bunge kwa miezi kumi kwamba limezua mtafaruku na mahusiano mabaya kwa wabunge wa pande zote mbili.

“CHADEMA walitafakari kwa kina udhalilishaji na uonevu waliofanyiwa wabunge wao na Mahakama ndio sehemu ya pekee ya kupata haki yao.

“Haijawahi kutokea Mbunge kusimamishwa vikao mwaka mzima kwenye uongozi wa Serikali za awamu zote zilizopita hapo nyuma, lakini serikali hii ya awamu ya tano imeweka historia,” alisema.

Aliahidi kutoa ushirikiano kwa wabunge ili kupata ufumbuzi wa tatizo hilo kwa sababu limeota mizizi kwa muda mrefu. Alisema viongozi wa chama tawala wanejaribu kuwanyanyasa wabunge wa upinzani kwa kisingizio cha kutumia kanuni.

Mbunge wa jimbo la Bunda, Esther Bulaya alisema kuwa watakwenda Mahakamani kupinga maamuzi dhalimu yaliyotolewa kwa wabunge wa upinzani Bungeni.

“Kama wanafikiri wataweza kutunyamazisha katika majimbo yetu wamekosea na hilo haliwezekani. Cha msingi sisi tunataka utu, haki na Demokrasia ya kweli itamalaki ndani na nje ya Bunge,” alisema.

Kwa upande wake, Halima Mdee alisema kuwa watafungua shauri Mahakamani na watapitia ushahidi ili kujiridhisha kama wana makosa ndipo watoe maamuzi kulingana na kosa lenyewe. Alisema kuwa polisi waliomtoa Mnyika Bungeni wameondolewa na kuletwa wengine kwa sababu ‘hawakumshughulikia’ Mnyika ipasavyo. Alisema kuwa Watanzania wote waliotazama video ile wakati Mnyika akitolewa Bungeni imetoa taswira ya namna gani Mbunge huyo alivyodhalilishwa kwa kiwango cha juu.



ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

Related Posts

Post a Comment