POLISI Waua Majambazi Matatu Katika Vita ya Majibizano ya Risasi Iliyoshangaza Watu Mwanza..!!!

WATU watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wameuawa kwa risasi jijini Mwanza jana katika kile kinachoelezwa kuwa ni matokeo ya vita kali ya kurushiana risasi baina ya watuhumiwa hao na askari wa Jeshi la Polisi.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alisema tukio hilo limetokea katika eneo la viwanja vya ST. Mary’s Mtaa wa Ndofe wilaya ya Nyamagana, ambako polisi walikuwa wameweka mtego baada ya kupata taarifa kuwa watuhumiwa walipanga kufanya uhalifu.

Ilielezwa zaidi kuwa polisi waliwafikia watuhumiwa baada ya kumkamata mganga wa kienyeji aitwaye Ayubu Nyamweru (45), mkazi wa Katoro mkoani Geita, ambaye alikutwa akiwa na kompyuta mpakato tatu na simu moja aina ya Sumsung vilivyokuwa imeibwa katika tukio la kuvunja nyumba maeneo ya Nyamanoro.

Tukio la kuporwa kwa vitu hivyo lilihusisha pia kuporwa kwa bastola aina ya Duty CZ 75P-07 na fedha, siku ya Mei 13 mwaka huu na kufunguliwa jalada lenye namba NY/IR/3773/2017.

Ilielezwa na polisi kuwa baada ya mganga Nyamweru kuhojiwa, alitaja wenzake anaoshirikiana nao katika kufanya matukio mbalimbali ya uvunjaji na unyanga’anyi jijini Mwanza na maeneo ya jirani.

Ilielezwa kuwa kufuatia maelezo ya mganga huyo, ndipo polisi walipofuatilia na kumkamata mtuhumiwa mwingine (Benedicto Thobias) kabla ya kuweka mtego uliosababisha kutokea kwa majibizano ya risasi baina yao na majambazi hao.

Akizungumza jana, Kamanda Msangi aliwataja watuhumiwa wlaiofariki kwa kupigwa risasi katika mapambano hayo kuwa ni Benedicto Thobias ambaye ni mkazi wa Nyamatara Buhongwa na wengine waishio pia Mwanza ni Mabula Segeja na Charles Thomas.

“Mnamo Mei 19 mwaka huu, katika viwanja vya ST. Mary’s mtaa wa Ndofe wilaya ya Nyamagana walifika watu watano ambao walikuwa ni wenzake na mtuhumiwa Benedicto. Askari walipowaamuru wajisalimishe walikaidi amri hiyo na kuanza kufyatua risasi uelekeo wa askari,” alisema Msangi na kuongeza:

“Ndipo askari wakajibu mapigo na kuwajeruhi majambazi wawili na zile risasi walizozipiga ziliweza kumjeruhi mwenzao (Benedicto) aliyekuwa amewapeleka askari kwenye eneo lile… wote watatu walifariki dunia wakati wanapelekwa hospitali kwa matibabu.”

Aidha, Kamanda Msangi alisema kuwa katika tukio hilo, polisi walifanikiwa kukamata silaha mbili ambazo ni bastola aina ya Duty CZ 75P -07 yenye namba B.512637 ikiwa na risasi 15 na magazini mbili na short gun iliyofutika namba ikiwa na risasi mbili na maganda mawili ya risasi, mali ya Suleimani Waziri aliyekuwa akiimiliki kihalali.

Kwa mujibu wa Kamanda Msangi, miili ya watuhumiwa hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa ajili ya uchunguzi na utambuzi zaidi wakati msako wa kuwasaka wenzao waliotoroka na wengine waliokuwa wakishirikiana nao bado ukiendelea.

Credit - Nipashe

Related Posts

Post a Comment