Kimenukaaa...Wanasheria Wajitokeza Kumpinga Makonda....!!!

BAADA ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kusema aliyekuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, hakuwa na mamlaka ya kuunda kamati kuchunguza tukio lake la kuvamia kituo cha Clouds Media, wanasheria nchini wamesema kiongozi huyo anapotosha umma.

Wamesema kauli ya Mkuu huyo wa Mkoa kuwa ana mamlaka sawa na waziri kutokana na kuteuliwa na Mamlaka moja ya uteuzi si sahihi, wakibainisha kuwa licha kuwa wakuu wa mikoa huteuliwa na Rais kama ilivyo kwa mawaziri, Nape aliunda kamati kuchunguza tukio lililotokea katika eneo linalosimamiwa na wizara yake, na si kuchunguza mwenendo na utendaji kazi wa Mkuu wa Mkoa.

Kiongozi huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam alitoa kauli hiyo juzi, wakati akihojiwa na kituo cha luninga cha Star Tv kwenye kipindi cha Tuongee Asubuhi, huku akikwepa baadhi ya maswali kuhusu elimu yake na jina lake halisi kwa kivuli cha “kuandamwa na wauza dawa za kulevya”.

“Hata kwa akili ya kawaida tu, unaweza kutofautisha mamlaka zao. Mkuu wa Mkoa ni kiongozi wa mkoa tu, ila waziri ni kiongozi wa nchi nzima kwa eneo analosimamia au kuongoza,” alisema Profesa Abdallah Safari.

Katika kipindi hicho, Bashite aliponda uamuzi wa Nape kuunda kamati ya kumchunguza baada ya kuvamia ofisi za Clouds Tv, akiwa na askari wenye silaha za moto na kulazimisha sehemu ya kipindi cha Shilawadu kurushwa hewani.

“Matukio kama haya hutokea nchi inapotaka kupinduliwa, lakini kama Rais yupo na nchi haijapinduliwa, basi kuingia ndani ya chombo cha habari na silaha, huku ni sawa na kunajisi uhuru wa habari,” alisema Nape.

Wakati akipokea ripoti ya kamati hiyo baada ya kupita saa takribani 24, Nape alisema ataifikisha kwenye Mamlaka za Uteuzi juu yake kwa maelezo kuwa yeye hana mamlaka ya kumchukulia hatua Mkuu wa Mkoa.

Hata hivyo, Nape aliachwa katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais John Magufuli saa 12 baada ya kupokea ripoti hiyo iliyokuwa na timu ya watu sita.

Wanasheria

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk James Jesse alisema: “Nape hakuandaa mamlaka ya kumchunguza Makonda, yeye alichunguza jambo lililotokea katika wizara yake, alichunguza jambo si mtu.

“Kama angemchunguza Mkuu wa Mkoa, kweli angekuwa hana mamlaka hayo. Lile ni tukio na ili upate picha ni lazima uhoji watu wote ambao walihusika kwenye hilo tukio,” alisema.

Kuhusu mamlaka zao, alisema: “Katiba haisemi kuhusu mamlaka, lakini ukitazama tu, mmoja anaongoza wizara ambayo ni mamlaka ya kitaifa na huyu mwingine anaongoza mkoa. Hivi utasema wote wanalingana kwa mamlaka kweli?”

Alisema ukubwa au mamlaka ya kiongozi hayatokani na ukubwa wa bajeti aliyonayo katika eneo analoongoza, “watu huangalia unaongoza mkoa, wilaya au wizara.”

Katika ufafanuzi wake, Profesa Safari alisema: “Kazi zao zinatofautiana sana. Waziri ni wa nchi nzima na mkuu wa mkoa ni wa mkoa tu. Waziri ni mjumbe wa Baraza la Mawaziri na katika kutekeleza wajibu wake, waziri ana wajibu wa kuunda tume kuchunguza jambo chini ya wizara yake.”

Aliongeza: “Kama huyo mkuu wa mkoa hataki kukubali kuhusu mamlaka ya waziri sijui anawaza nini, maana hili liko wazi na wanasheria tumelieleza kiundani zaidi. Kama hatambui hilo anashangaza, huko ni kujinyanyua tu.”

Alisema Nape alikuwa na lengo la kutaka kujua ukweli wa tukio lililotokea Clouds Tv, na si kumchunguza mkuu wa mkoa.

Mhadhiri mwingine wa Chuo hicho, Dk Onesmo Kyauke huku akichambua sheria inayoongoza utendaji katika mikoa (The Regional Administration Act), alisema waziri anaweza kutoa mapendekezo dhidi ya mkuu wa mkoa kwa Mamlaka ya Uteuzi ambayo ni Rais.

“Kama mkuu wa mkoa akifanya kosa, nafikiri waziri anapaswa kuwasilisha malalamiko yake kwa Rais… mkuu wa mkoa anashughulikia mkoa wake tu, lakini waziri anashughulikia majukumu yanayohusu wizara yake kitaifa, yaani nchi nzima, ila tatizo ni kuwa mkuu wa mkoa hayuko chini ya waziri.”

Katiba

Kwa mujibu wa Ibara ya 61 (2) ya Katiba ya Tanzania; wakuu wa mikoa Tanzania Bara watateuliwa na Rais baada ya kushauriana na Waziri Mkuu.

Kifungu kidogo cha (4) kinasema; Bila kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (5), kila Mkuu wa Mkoa, atakuwa na wajibu wa kusimamia utekelezaji wa kazi na shughuli zote za Serikali ya Jamhuri ya Muungano katika mkoa aliokabidhiwa; na kwa ajili hiyo, atatekeleza kazi na shughuli zote zilizotajwa na sheria, au kwa mujibu wa sheria kama hizi au shughuli za mkuu wa mkoa na atakuwa na madaraka yote yatakayotajwa na sheria yoyote iliyotungwa na Bunge.

Mawaziri

Ibara ya 55 (1) inasema; Mawaziri wote ambao ni wajumbe wa Baraza la Mawaziri kwa mujibu wa ibara ya 54 watateuliwa na Rais baada ya kushauriana na Waziri Mkuu.

Kifungu kidogo cha (2) kinasema; Pamoja na mawaziri waliotajwa katika ibara ndogo ya (1), Rais aweza, baada ya kushauriana na Waziri Mkuu, kuteua naibu mawaziri. Naibu mawaziri wote hawatakuwa wajumbe wa Baraza la Mawaziri.

(3) Rais aweza kuteua idadi yoyote ya naibu mawaziri ambao watawasaidia mawaziri katika utekelezaji wa kazi na shughuli zao. (4) Mawaziri na naibu mawaziri wote watateuliwa kutoka miongoni mwa Wabunge.

(5) Bila kujali masharti ya ibara ndogo ya (1), ikitokea
kwamba Rais anahitajika kuteua waziri au naibu waziri baada
ya Bunge kuvunjwa, basi aweza kumteua mtu yeyote ambaye
alikuwa mbunge kabla ya Bunge kuvunjwa.

Related Posts

Post a Comment